Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Sheria ya Ushindani ya mwaka 2024 ni kumlinda mlaji.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo(Mb) amesisitiza kuwa lengo la marekebisho ya Sheria ya Ushindani ya mwaka 2024 ni kumlinda mlaji.

Amesema lengo la mabadiliko hayo si adhabu bali ni kuleta hamasa kwa watumiaji ambapo eneo kubwa limeelekezwa kwenye elimu ili watanzania ambao ni walaji waifahamu.

Hayo ameyasema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viunga vya bunge mara baada ya kupitishwa kwa muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya ushindani ya mwaka 2024.

“Mjadala umekuwa mzuri tumekuwa na muswada wa sheria ya Tume ya Ushindani(FCC) ambao lengo lake lilikuwa ni kumjali mteja hasa upande wamiliki wa hodhi wa soko kutoka asilimia 35 hadi 40,”amesema.

Amesema maeneo mengine yameakisi ni jinsi gani mlaji anapata faida kubwa ili kuhakikisha hazuiwi kupata bidhaa stahiki katika eneo lake bila kudhulumiwa.

Aidha, amesema pia kulikuwa na suala la kupanga 'kudisplay' bei kwa wateja ambapo bunge limeshauri kitumike kifungu cha awali na kutumia utaratibu wa mwanzo bila kuweka adhabu ikiwezekana yafanyike maboresho kwa lengo la kutekeleza sheria kwa ufasaha na wafanyabiashara kuzingatia matakwa ya sheria inavyotaka.

“Tunashukuru maelekezo ya bunge yameenda vizuri na muswada umepita hivyo tunasubiri Rais aweze kuusaini ili kuwa sheria kamili.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio amesema hiyo ni ya muda mrefu na kwamba marekebisho hayo yatawawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo ya serikali ya awamu ya sita ya kuvutia biashara na kumlinda mlaji.

“Marekebisho yaliyofanyika ni mengi ikiwemo kubadilisha vifungu vya ushindani, na kuruhusu tume kutoa adhabu katika makosa yanayomuathiri mlaji ambapo vifungu vingine havikuwepo mwanzo, tunaishukuru serikali kwa maboresho haya yakianza kutumika tutatoa elimu ili watu waelewe zaidi,”amesisitiza.