Habari
WANAFUNZI NA WAVUMBUZI WACHANGA WASHAURIWA KUTUMIA MAJUKWAA YA BIASHARA
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Aristides Mbwasi ametoa rai kwa Wanafunzi na Wavumbuzi wachanga kutumia majukwaa mbalimbali ya biashara ili kujifunza, kuungana, na kujaribu mawazo mbalimbali ya biashara na ujasiriamali kama Siku ya Chuo Kikuu cha Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali.
Amesema hayo wakati anamwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Judith Kapinga wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mzumbe pamoja na Kambi ya Ujasiriamali yaliyofanyika katika Ukumbi wa Samora, Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro, Mei 08, 2026.
Bw. Mbwasi amesema kuwa majukwaa kama hayo yanawaleta pamoja wajasiriamali wachanga, wanafunzi, wavumbuzi, na wadau wa biashara kwa kushirikiana na Serikali, Vyuo vikuu, Sekta binafsi, washirika wa maendeleo, na vituo vya uvumbuzi kwa kufanya kazi kwa pamoja ambapo mawazo hubadilishwa kuwa bidhaa na huduma zinazofaa.
Aidha ameongeza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara, inaendelea kuunga mkono mipango inayokuza ujasiriamali na maendeleo ya viwanda kwa kuendelea kuboresha sera na kanuni zinazowezesha biashara kukua, kurahisisha taratibu za uwekezaji na biashara, na kutengeneza uhusiano imara zaidi Kupitia programu za maendeleo ya biashara ndogo na za kati, juhudi za urasimishaji wa biashara, maonyesho ya biashara, na usaidizi wa kuongeza thamani na kufungua fursa kubwa zaidi kwa Watanzania hasa vijana na wanawake kuanzisha na kupanua biashara.
Vilevile Bw.Mbwasi ameongeza kuwa Wizara pia inafanya kazi kwa karibu na taasisi za fedha, taasisi za mafunzo, na washirika wa maendeleo ili kupanua upatikanaji wa fedha, ujuzi wa ujasiriamali, uhamisho wa teknolojia, na masoko ya ndani na kimataifa ambapo Jitihada hizo zinachangia moja kwa moja katika utekelezaji wa Dira ya Tanzania ya 2050 kwa kujenga sekta binafsi yenye uthabiti na ushindani.
Pia ametoa rai kwa washirika na wadau kuendelea kuwekeza katika wajasiriamali wachanga kwani Ushauri wao, ufadhili, na ushirikiano unaweza kuharakisha kwa kiasi kikubwa ukuaji wa mawazo bunifu kuwa biashara zenye tija
