Habari
TANZANIA, AUSTRIA KUMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA NA UWEKEZAJI WA VIWANDA
Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Austria zimejadili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, kwa lengo la kufungua fursa mpya za kiuchumi na kukuza sekta ya viwanda nchini.
Majadiliano hayo yamefanyika, Machi 23, 2026, kati ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Mhe. Balozi Hannah Liko, yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo, yamehusu kuelekeza nguvu katika uanzishaji wa uwekezaji wa kuongeza thamani ya bidhaa ghafi, kukuza uhaulishaji wa teknolojia, pamoja na kupanua wigo wa masoko ya bidhaa za Tanzania nchini Austria.
Pamoja na hayo, viongozi hao wamejadiliana kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na anga kama kichocheo cha kurekebisha urari wa biashara, hatua inayotajwa kurahisisha ufanyaji biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande mwingine, Londo na Balozi Liko wamejadiliana kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Austria kwa Afrika 2026–2029, utakaolenga kuimarisha uwekezaji wa kampuni za Austria nchini Tanzania kupitia mifumo ya kupunguza hatari za kibiashara.
Londo amebainisha kuwa Tanzania inachukulia ushirikiano huo kama fursa ya kimkakati na lango muhimu la kuimarisha uwezo wa Viwanda na Biashara Ndogo na za Kati – SMEs, kufikia viwango vya soko la Ulaya na hivyo kuvutia biashara na uwekezaji nchini.
