Habari
TANZANIA YASISITIZA MASUALA MUHIMU KATIKA KUBORESHA SHIRIKA LA BISHARA LA DUNIA (WTO)
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshiriki kikamilifu katika Mkutano wa 14 wa Mawaziri wa Biashara unaofanyika kuanzia tarehe 26 - 29 March 2026.
Kupitia Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Habiba Hassan Omar amemwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga(Mb).
Dkt Habiba alisisitiza kuhusu umuhimu wa Biashara ya Kidijitali kuwa moja ya nyenzo muhimu katika kutengeneza ajira na kukuza Uchumi kwa nchi mbalimbali.
Aidha, Dkt. Habiba amesisitiza kuwa Biashara chini ya Shirika la Biashara Duniani imeendelea kusimamiwa chini ya mikataba ya kimataifa ya WTO. Licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi na migogoro ya kijiographia bado biashara ya kimataifa imeendelea kukua mwaka hadi mwaka. Mfano;-
Biashara ya bidhaa imeendelea kukua kutoka dola za Marekani Trilioni 5 mwaka 1995 mpaka Trilioni 25 mwaka 2023; Biashara kwa ujumla imekuwa mara tano zaidi tangu kuanzishwa kwa WTO mwaka 1995; Wastani wa Ushuru umeendelea kupungua kutoka asilimia 10 - 15 kabla ya mwaka 1995 mpaka asilimia chini ya 7 kwa sasa; na Kwa nchi zilizoendelea ushuru umebaki kuwa chini ya asilimia 4 na hivyo kuonesha hatua kubwa kwenye biashara ya Kimataifa.
Aidha, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuthibitisha tena dhamira yake ya kuunga mkono mfumo wa biashara wa kimataifa ulio wa haki, jumuishi, uwazi na unaozingatia maendeleo chini ya WTO. Tunasimama pamoja na nchi zinazoendelea na zile zilizo katika kundi la nchi zenye Uchumi Mdogo (LDCs) na kusisitiza umuhimu wa matokeo yanayoleta mabadiliko halisi ya kiuchumi na ustawi wa pamoja.
Dkt Habiba ameongeza kuwa baadhi ya masuala yanayojadiliwa yanasisitiza kwamba, maendeleo yanapaswa kubaki kiini cha majadiliano yote. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa masharti ya Upendeleo Maalum kwa nchi zinazoendelea ili kuhakikisha tunapata nafasi ya kutosha ya kusimamia na kutekeleza Sera za kukuza viwanda, kuongeza thamani ya bidhaa zetu, na kuimarisha uchumi wa Taifa.
