Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Tanzania iko tayali kuwapokea na kuwahudumia wawekezaji na wafanyabiashara  kutoka Umoja wa Ulaya.


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amesema Tanzania iko tayali kuwapokea na kuwahudumia wawekezaji na wafanyabiashara  kutoka Umoja wa Ulaya kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali pamoja na miradi ya kimkakati kwa kuwa Tanzania ina mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara.Waziri Kijaji ameyasema hayo  Februari 24, 2023 wakati wa majadiliano na wafanyabiashara waliotoka katika nchi 27 za Umoja wa Ulaya walioshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya lililofanyika tarehe 23 na 24 Februari, 2023  JNICC, Dar es Salaam.

Akiwa pamoja na Viongozi wa Wizara wakiwemo Naibu Waziri Mhe. Exaud Kigahe, Katibu Mkuu  Dkt. Hashil Abdallah, Naibu Katibu Mkuu Bwana Ally Gugu, Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji Bwana Fadhil Chilumba  walisikiliza na kujibu hoja na maswali yote ya wafanyabiashara hao wenye nia ya kuwekeza Tanzania.

Nao Wakuu wa Taasisi za  Kituo cha Uwekezaji (TIC) Bwana Gilead Teri, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya uzalishalishaji kwa mauzo ya nje (EPZA) Bw. Charles Itembe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dr. Nicolaus Shombe na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzanina (TANTRADE) Bi. Latifa Mohamed Khamisi  walieleza taratibu zote zinazotakiwa kufuatwa na mwekezaji yeyote kupitia taasisi zao na kutangaza maeneo ambayo yako tayari kwa uwekezaji  zikiwemo kongani za viwanda na miradi ya kimkakati.

Naye Katibu  Mtendaji wa  Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Dkt. Godwill Wanga aliwahakikishia Wafanyabiashara hao kuwa Baraza hilo ambalo Mwenyekiti wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liko tayari kushughulikia hoja zitakazojitokeza kupitia  Mabaraza ya Biashara yaliyopo katika kila Mkoa na Halmashauri.

Vilevile, Wafanyabiashara hao kutoka kampuni mbalimbali zilizopo Umoja wa Ulaya walipata fursa ya kuuliza masuala mbalimbali kuhusu maeneo na taratibu za kuwekeza nchini  na kujibiwa na kupatiwa utaratibu wa kuja kuwekeza nchini kupitia TIC.