Habari
Tanzania imekubaliana na vigezo vya uasili wa bidhaa ambavyo havitaathiri bidhaa zinazozalishwa nchini

Tanzania imekubaliana na vigezo vya uasili wa bidhaa ambavyo havitaathiri bidhaa zinazozalishwa nchini kwenye maeneo maalum na nje ya maeneo maalum ya uzalishaji wa bidhaa kwa mauzo ya nje.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bw. Omar Shaaban akimwakilisha Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Ashatu Kijaji, katika Mkutano wa 11 wa Mawaziri wa Biashara wa Eneo Huru la Biashara Afrika uliofanyika Februari 11-12 , 2023.
Waziri Shaban ameongoza ujumbe kutoka Tanzania uliojumuisha Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Exaud Kigahe(Mb), Naibu Katibu Mkuu-Uwekezaji, Bw Ally Gugu, pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Mipango, EPZA na TRA.
Aidha, wakati wakishiriki Mkutano huo, Viongozi hao walilenga kutetea maslahi ya TAIFA hususan katika upatikanani wa fursa ya soko ikiwemo la nguo na mavazi uunganishaji wa magari; na kuweka utaratibu maalum wa biashara ya bidhaa zinazozalishwa katika maeneo maalum ya uzalishaji kwa ajili ya kukuza mauzo nje ya nchi.
Vilevile, Viongozi hao wamejipa muda zaidi wa kufanyia kazi na kupata ushauri zaidi kwa wadau kabla ya kukubaliana na vigezo vya kuruhusu biashara katika Sekta ya nguo na mavazi na uunganishaji wa magari ambazo ni mojawapo ya Sekta muhimu katika kukuza biashara, kuongeza fursa za ajira na mapato katika Bara la Afrika kupitia AfCFTA.
Mkutano huo ni sehemu ya Maandalizi ya Mkutano wa Nchi na Serikali wa UMOJA wa Afrika ambao unatarajiwa kupokea taarifa na kufanya uamuzi kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).