Habari
Tanzania Kufanya Biashara chini ya Mkataba wa AfCFTA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu amesema, Tanzania iko tayari kufanya biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Bara la Afrika( AfCFTA)
Ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) uliolenga kuhamasisha Sekta Binafsi kuhusu Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) katika utekelezaji wa Itifaki ya Biashara ya Bidhaa uliofanyika Februari 15, 2023 jijini Dar es Salaam.
"Warsha hii ni moja ya juhudi za muendelezo wa Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi katika kuwaelimisha Watanzania hususan wafanyabiashara na wawekezaji nchini kuhusu fursa zilizopo ndani ya nchi na AfCFTA " Amesema Bw. Gugu
Aidha, Bwana Gugu amewapongeza Wafanyabiashara waliochangamkia fursa kwa kushirikiana na kuchangia Tanzania kuingiza kwa kuuza zaidi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuuza zaidi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC.
Aidha amesema kuwa fursa hizo zinapaswa kuongezwa ili kusaidia Wafanyabiashara kuendelea kupata masoko na kuuza bidhaa zao katika soko kubwa la Afrika.
"Nafasi yetu kama Tanzania kwa sasa kuuza Afrika bado iko chini, tuseme kwa ujumla wake na tunadhani kwa kupitia takwimu au chambuzi ambazo zimefanyika na wenzetu wa Benki ya Dunia, AfCTA itanyayua zaidi ya Waafrika Milioni 60 kutoka kwenye Umaskini "
Kwa upande wake Balozi wa Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC) Raphael Maganga amesema Serikali inapaswa kuteleleza mikakati yake katika kuhakikisha Biashara ya Tanzania na Afrika inakuwa kwa kubwa zaidi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Nebart Mapwele amesema uwepo wa Mkataba wa AfCFTA utaleta fursa kubwa kwa wafanyabisahara na kukuza uchumi nchini.
"Kuna fursa kubwa sana katika kufanya biashara Afrika nasisi kama TCCIA tuko bega kwa bega kushirikiana na wenzetu kuhakikisha kwamba hizi biashara zinafanyika, na vibali tumeshaviandaa viko tayari,hivi vibali vitasaidia kwa mfanyabiashara kwenda kupata unafuu wa kodi" Amesema Bwana Mapwele.