Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA ISIBAKI MTAZAMAJI KATIKA SOKO LA AFCFTA LA WATU BILIONI 1.4


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Mbwasi, amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za masoko ya kikanda ili kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Afrika.

Mbwasi amesema hayo Julai 15, 2026 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Judith Kapinga (Mb), wakati akifungua mafunzo ya uhamasishaji wa sekta binafsi kuhusu fursa za biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).

Amesema masoko hayo ni fursa kubwa kwa wazalishaji wa Tanzania, kwani AfCFTA linaunganisha nchi 54 zenye watu zaidi ya bilioni 1.4 na uchumi unaozidi Dola za Marekani trilioni 3.4, huku EAC na SADC yakiwa na mamilioni ya walaji wanaohitaji bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Fursa hii ni kubwa, Tanzania haipaswi kubaki mtazamaji katika soko hili, bali wafanyabiashara wanapaswa kujipanga na kutumia fursa zilizopo,” amesema.

Ameeleza kuwa tayari kuna mafanikio katika biashara ya kikanda, ambapo mauzo ya Tanzania katika soko la SADC yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 2.97 mwaka 2024 hadi bilioni 3.55 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 19.4.

Hata hivyo, amesema ni kampuni 40 pekee za Tanzania zilizotumia Vyeti vya Uasili wa Bidhaa vya AfCFTA hadi Aprili 2026, hivyo akatoa wito kwa wafanyabiashara wengi zaidi kutumia fursa hiyo.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia taasisi zake ikiwemo TanTrade, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), SIDO na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TISEZA), ili kuwawezesha wafanyabiashara kuingia katika masoko mapya ya kikanda.