Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Tanzania na Finland kuendeleza uhusiano wa kibiashara na uwekezaji


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania itaendeleza uhusiano wa uwekezaji na biashara na nchi ya Finland ili kukuza uchumi wa nchi zote mbili na watu wake.

Waziri Kijaji ameyasema hayo Januari 31, 2023 alipokutana na kuzungumza na Waziri wa Uchumi wa Finland Mhe. Mika Tapani Lintila, aliyeambatana na Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji 18 kutoka nchini humo, Ofisi za Wizara, Dodoma.

Katika Mkutano huo, Waziri Kijaji alieleza fursa mbalimbali za uwekezaji na ufanyaji biashara Tanzania pamoja na utayari wa kupokea wawekezaji wakati Waziri lintila alieleza utayari wa wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuwekeza hapa nchini.

Aidha, wafanyabiashara na wawekezaji walioambatana na Waziri huyo walionesha utayari wa kuja kiwekeza Tanzania katika sekta za elimu, teknolojia, nishati, madini, ujenzi na TEHAMA ambazo wana ujuzi na uzoefu mkubwa nazo.