Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Tanzania na Malawi kukuza uhusiano wa kibiashara  na uwekezaji


Tanzania na Malawi kukuza uhusiano wa kibiashara  na uwekezaji

Tanzania na Malawi zimekubaliana kukuza uhusiano wa kibiashara  na uwekezaji  kwa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji  baina ya nchi hizo ikiwemo uboreshaji wa sheria  za uwekezaji, ukamilishaji wa ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Kasumulo  na  huduma za  Bandari ya Mbamba Bey ili kukuza biashara na uchumi katika nchi hizo.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah Aprili 26, 2023 kwa niaba ya  Waziri  wa Wizara hiyo Dkt. Ashatu Kijaji  alipokuwa akihutubia Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi  linalofanyika 26 - 29/04/2023 Mzuzu Malawi.

Aidha, amesema Tanzania inawakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Malawi  kuja kuwekeza na kufanya biashara Tanzania katika sekta za kilimo, uvuvi, uchumi wa bluu, uzalishaji utalii, huduma  za fedha, uchukuzi, miundombinu, mawasiliano, madini elimu na afya ili kukuza biashara na uchumi wa nchi hizo

Vilevile amewataka wafanyabishara na wawekezaji wa Tanzania kutumia   kikamilifu fursa zinazopatikana  baina ya nchi hizo  kulingana na raslimali zilizopo katika nchi hizo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara  ambayo imefikia  kiasi cha  dola za Marekani milioni 86.7 mwaka 2022. 

Naye Waziri wa Biashara na Viwanda wa Malawi Mhe. Simplex Chithyola Banda (Mb.)  amesema Malawi iko tayari kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya nchi hizo uliopo tangu  Uongozi wa  Serikali ya Awamu ya kwanza ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini humo. 

Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Msaada wa chakula na vifaa vya kujihifadhi  alioutoa wakati Malawi ilipokumbwa  na kimbunga freddy Machi 2023

Kwa upande wa  Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Humprey Polepole amesema kongamano hilo limewakutanisha wafanyabiashara  na wawekezaji  zaidi ya 300 kujadili, na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika  biashara zao baina ya nchi hizo. 

Pia amewashauri watanzania kuwa wabunifu na kushirikiana na wafanyabiashara wa Malawi kutumia fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Malawi ambayo ni moja ya nchi sisizokuwa  na bahari