Habari
Tanzania na Zambia zakubaliana kutatua changamoto za kibiashara

Tanzania na Zambia zimekubaliana kutatua changamoto 8 kati ya 24 za kibiashara na 16 zilizobaki zimewekewa utaratibu wa kuzitatua ifikapo Disemba 31, 2023 ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya Tanzania na Zambia ikiwemo kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah Oktoba 10, 2023 akiongea na vyombo vya habari wakati wa Mkutano wa Pamoja wa Kujadili Changamoto za Biashara kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika 09 - 10/10/2023 katika Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani- Tunduma, Songwe.
Aidha, Dkt. Abdallah amesema nchi hizo zimekubaliana kuwa bidhaa zinazosafirishwa kutoka Tanzania kwenda nchi nyingine kupitia Zambia zikiwa na vibali vyote vinavyohitajika ziruhusiwe kupita nchini humo kwenda nchi husika bila kizuizi kulingana na Makubaliano ya Kibiashara ya ya WTO na SADC.
Vilevile, amezitaka Taasisi zote za umma zinazohusika na utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara wa huduma ya usafirishaji baina ya nchi hizo kuhakikisha hawawakwamishi bila sababu za msingi bali kuwasaidia kutatua changamoto zao hususani upatikanaji wa vibali kulingana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo katika makubaliano ya kibiashara chini ya Makubaliano ya Kibiashara ya WTO na SADC.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zambia, Bi. Lillian Bwalya amesema nchi ya Zambia imekubali kutatua changamoto hizo ili kurahisisha na kukuza biashara za mpakani baina ya nchi hizo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amesema makubaliano hayo ni muhimu katika kutatua changamoto mbalimbali baina ya nchi hizo hususani katika kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma unaopotisha asilimia 80 ya mizigo kutoka Bandari ya Dar es salaam kwenda nchi za kusini mwa Afrika zisizo na bahari.