Habari
TANZANIA IKO TAYARI KWA WAFANYABIASHARA NA WAWEKEZAJI KUTOKA OMAN

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah alisema Kuwa Serikali ya Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisheria ili kuvutia Wafanyabiashara na Wawekezaji wa ndani na nje.
Aliyasema hayo Septemba 08, 2025 wakati akifungua Mkutano wa Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman waliotembelea nchini kwa lengo la kukuza ushirikiano katika sekta za biashara na viwanda.
“Tanzania iko tayari kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Oman. Tunayo ardhi yenye rutuba, rasilimali za asili, soko la ndani na kikanda, amani na utulivu wa kisiasa, pamoja na watu wakarimu. Tunaamini kwa kushirikiana, tunaweza kufanikisha malengo ya pamoja ya maendeleo ya kiuchumi.”Amesema Dkt. Abdallah
Aidha, Dkt. Abdallah alibainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), biashara kati ya Tanzania na Oman imeendelea kukua, ikionyesha ongezeko kubwa kutoka Dola za Marekani milioni 18 mwaka 2017 hadi kufikia Dola milioni 245.8 mwaka 2024.
Vilevile, albainisha kuwa uuzaji wa bidhaa za Tanzania kwenda Oman umeongezeka kutoka Dola milioni 4.8 mwaka 2017 hadi Dola milioni 16.5 mwaka 2024.
Dkt Abdallah pia alizitaja bidhaa zinazouzwa Oman kutoka Tanzania kuwa ni pamoja na nyama ya mbuzi, kaa, mbegu za mboga, kahawa, mahindi, maharage, na juisi mbalimbali. Bidhaa zinazoingia nchini kutoka Oman ni mafuta ya petroli, mbolea za kemikali, saruji, maziwa, na vifaa vya umeme kama transfoma.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli alisema sekta muhimu ambazo wanaweza kuwekeza ni pamoja na mafuta ya kula, ngano, matunda na mbogamboga.
Naye, Mjumbe wa Baraza la Nchi na Mwenyekiti wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Oman Mkoa wa Al Wusta na Kiongozi wa Ujumbe huo Dkt. Salem bin Salim Al-Junaibi alisema chemba za wafanyabiashara za nchi zote mbili, zinalenga kusaini mikataba ya uwekezaji itakayochochea maendeleo na kunufaisha nchi zote mbili.