Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA ITAENDELEA KUPOKEA UWEKEZAJI MKUBWA KUTOKA CHINA


Tanzania itaendelea kupokea na kulinda uwekezaji mkubwa kutoka China kwa kuwa ina mazingira rafiki, Sera wezeshi, na fursa lukuki katika sekta ya viwanda na biashara.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga Machi 20, 2026 wakati akizindua ziara yake ya kimkakati ya siku tatu nchini humo, inayolenga kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kuvutia mitaji ya kigeni itakayochochea ukuaji wa viwanda nchini Tanzania.

Waziri Kapinga ameanza ziara hiyo jijini Hangzhou, katika Jimbo la Zhejiang, ambapo ameshiriki kongamano la wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Kampuni takribani 100 lililoratibiwa na Baraza la China la Kukuza Biashara ya Kimataifa (CCPIT) – Kamati ya Jimbo la Zhejiang.

Katika kongamano hilo, Waziri amewasilisha vivutio vya uwekezaji vilivyopo nchini, akisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na Jimbo la Zhejiang, hususan katika sekta za uzalishaji na teknolojia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la China la Kukuza Biashara ya Kimataifa (CCPIT) Jimbo la Zhejiang, Bw. Chen Jianzhong, amepokea kwa mikono miwili utayari huo wa Tanzania na kuahidi kuimarisha mahusiano ya kibiashara huku akibainisha Jimbo hilo liko tayari kuhamasisha wawekezaji wake kuja nchini Tanzania kuwekeza katika ujenzi wa viwanda ili kusaidia kuhamisha teknolojia na kuongeza thamani ya bidhaa za Kitanzania.

Ziara hii ya Waziri Kapinga, ambayo inajumuisha makongamano na vikao vya kimkakati vya ana kwa ana na wamiliki wa viwanda, inatarajiwa kuendelea katika Jiji la Fuzhou (Jimbo la Fujian) na kuhitimishwa jijini Huizhou (Jimbo la Guangdong) ambapo Matarajio ya ziara hiyo ni kuongeza idadi ya viwanda vipya nchini na kufungua masoko zaidi kwa bidhaa za Tanzania nchini China.