Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda ma Biashara Dkt.Hashil T. Abdallah akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo(Mb) ameongoza Ujumbe wa Tanzania kukutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,Uvuvi na Maji wa Serikali ya Oman Dkt. Ahmed Al Bakri Aprili 28 , 2025 katika Hoteli ya St.Regis Jijini Muscat Oman.
Mazungumzo hayo yamelenga kuendeleza sekta ya Kilimo nchini Tanzania na Oman ambapo kwa Tanzania Sekta ya kilimo ni muhimu sana katika uchumi ikichangia asilimia kubwa ya Pato la Taifa, ajira, na malighafi za viwanda.
Aidha Ushirikiano huo katika sekta hiyo ya kilimo utasaidia Mfumo wa Uwekezaji wa Ajenda 10/30 (2024-2030) unaotaka kuongeza ukuaji wa sekta hiyo hadi asilimia 10, ukihimiza ushirikiano na sekta binafsi pamoja na Programu ya BBT-YIA unaolenga kuwawezesha vijana na wanawake katika kilimo biashara kwa kuwapatia ardhi, mitaji, ujuzi, na masoko.
Vilevile Serikali ya Tanzania kupitia ujumbe huo umewakaribisha wawekezaji mbalimbali kutoka Oman kuwekeza katika Sekta ya Kilimo na kuhimiza ushirikiano na sekta binafsi hasa katika maeneo ya umwagiliaji, ushirika, mbegu, miundombinu ya hifadhi, kilimo kidijitali, masoko, kilimo endelevu, mifugo, viungo, na mazao ya bustani kwani Tanzania inalenga kujitosheleza kwa chakula na kuuza nje.
Mazungumzo hayo pia yaliyohudhuriwa na Balozi wa Tanzania Nchini Oman Mhe.Fatma Abdallah, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Nchini Tanzania Dkt.Stephen Nindi, Viongozi wa sekta binafsi na Maafisa kutoka Wizarani.