Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

KAMATI ITUSHAURI UWEKEZAJI WENYE TIJA KIWANDA CHA GENERAL TYRE- BALOZI SALUMU


Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe.Balozi Waziri Salum ameiagiza kamati ya wataalam itakayofanya uchambuzi na kushauri uendelezaji wa eneo la Kiwanda cha kutengeneza Matairi cha General Tyre kilichosimamisha uzalishaji tangu 2007 kilichopo Mkoa wa Arusha kushauri namna bora itakayofanya eneo hilo kutumika kwa usahihi pasipo kuondoa dhima na nia njema ya uanzishwaji wa kiwanda hicho na Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Julius Nyerere ya Serikali kupata mapato Pamoja na kutengeneza ajira kwa watanzania.
 
Ametoa agizo hilo alipohitimisha ziara yake ya kutembelea kiwanda cha General Tyre kilichopo Arusha na Kiwanda cha Kilimanjaro Machine tools (KMTC) kilichopo Mkoa wa Kilimanjaro Aprili 27,2026 ambapo amesema kama Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara itahakikisha inatathmini namna bora ya uwekezaji katika eneo hilo ikiwepo uwekezaji wa viwanda au uwekezaji wa biashara kulingana na mapendekezo ya kamati hiyo.
 
Aidha ameongeza kuwa ripoti ya kamati hiyo itatoa mwanga wa kumshauri Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga namna bora na aina ya uwekezaji kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 54 kulingana na mapendekezo ya kamati hiyo ikiendana na maono ya mwanzilishi wa Kiwanda hicho Hayati Julius Nyerere pamoja na kutunza historia yake.
 
Kwa upande wa Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools Balozi Salum amesema katika kuendeleza na kukipa nguvu kiwanda hicho Wizara itahakikisha kwenye Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 inatenga fedha za kutosha ili kuongeza mashine za kisasa zaidi ambazo zitapelekea vijana wengi wa Mikoa hiyo ya Kaskazini kujifunza na kupata ujuzi ambao wanaweza kutumia na kujiajiri.

Balozi Salum ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwafikia wamiliki wa Viwanda ambavyo havifanyi kazi kuanza kuvifufua ikiwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Saluhu Hassan ya kuhakikisha viwanda vyote vinafufuliwa ili vijana waweze kupata ajira kwenye viwanda hivyo.