Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUENDELEA KUFANIKISHA AJIRA KWA WATANZANIA


Serikali inaendelea kutengeneza fursa za ajira za Watanzania wengi kwa kuhamasisha Uwekezaji wa Viwanda vikubwa na tayari mafanikio yameanza kuonekana kutoka Sekta binafisi na Umma.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Abdallah Kilima wakati akiongozana na Ujumbe wa Wafanyabiashara kutoka nchini Omani walipotembelea Kampuni ya Sartun inayojishughulisha na uundaji na uunganishaji wa magari nchini Septemba 9, 2025 jijini Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi wa Sartun, Bw. Rehmatullah Habib, amesema kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuongeza ajira kwa Watanzania na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

"Matarajio yetu ni kufikia wafanyakazi 350 kutoka 250 tulionao sasa. Baadhi ya vijana wetu walipoanza kazi hawakuwa na ujuzi wowote, lakini sasa wanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa," alisema Bw. Habib.

Bw. Habib alieleza kuwa tangu uzinduzi wa kiwanda hicho mwaka jana, mauzo ya magari yameongezeka kutoka magari 200 hadi 1,800 kwa sasa.

Makamu wa Rais wa Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Oman (Oman Chamber of Commerce and Industry), Bw. Yagoob Al Rabaani alifurahishwa kuona kuwa Tanzania ina uwezo wa kuunganisha magari ya yenye ubora wa hali ya juu na kiwanda kizuri kilicho na viwango vya juu.
“Tunataka ushirikiano. Nchini Oman tuna maeneo ya free zone, hivyo tunaweza kushirikiana na pia kuhamishia teknolojia hii Oman ili kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu,” alisema Bw. Al Rabaani
"Tumefurahi kuona Tanzania ikiunganisha magari yenye ubora wa hali ya juu. Tuko tayari kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya pamoja ya teknolojia kati ya Oman na Tanzania," alisema

Naye Mkurugenzi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Juma Mwambapa, alisema serikali imekuwa na nia thabiti ya kuhamasisha uwekezaji wa viwanda na tayari imeshuhudia mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma.

Aidha, kiwanda cha Sartun kwa sasa kinafanya kazi katika *shifts* mbili badala ya tatu, kutokana na upungufu wa wafanyakazi, lakini kikikamilika kitaweza kutoa ajira kwa zaidi ya watu 250 kwa muda wa zamu tatu.