Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA ZA VIATU VYA NGOZI KWA WADAU WA SHULE


Serikali imesema itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ya viatu vya Ngozi kwa wadau mbalimbali wa shule.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Manongi Sempeho wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Viatu vya ngozi vya shule Tanzania akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hashil Abdallah ambaye ndiye aliyekuwa amealikwa kuwa Mgeni rasmi wa tukio hilo Septemba 2, 2025 jijini Dar es Salaam.

Sempeho ameongeza kuwa nchi inazaidi ya ng'ombe milioni 33 na mbuzi milioni 25 na endapo wazalishaji watatumia teknolojia nzuri na kufuata viwango vya ubora unaohitajika sokoni utasaidia kupunguza uagizaji wa jozi za viatu kutoka nje ya nchi.

Naye Mwenyekiti Msaidizi wa Bodi ya wadhamini wa Chama cha watengenezaji wa viatu vya ngozi- TALEPPA amesema kuwa Chama kinalenga kutengeneza jozi za viatu vya shule milioni 10 vyenye thamani ya shilingi bilioni 300 kwa mwaka hatua itakayowezesha sekta ya ngozi nchini kuendelea kukua , kuchangia pakubwa katika uchumi na kutoa ajira kwa watu zaidi ya milioni mbili

Hata hivyo, Katibu wa chama hicho Timoth funto anasema wamelenga soko la wanafunzi kwa kuwa ni rahisi kupenya akiweka wazi kuwa soko la bidhaa za ngozi nchini ni kubwa lakini soko limeendelea kuwa chini. Kutokana na miundombinu hafifu , teknolojia duni , wataalamu wenye ujuzi , sera na mazingira ya Ushindani yasiyo na usawa yamefanya bidhaa za ngozi za Tanzania kutokupenya kwenye soko la ndani na kimataifa.

Aidha, imewekwa wazi kuwa nchi huingiza bidhaa za ngozi takribani jozi za viatu milioni 54 kila mwaka huku uzalishaji wa bidhaa za ngozi ukiwa chini ya milioni tano kwa mwaka.