Habari
Wizara ya Viwanda na Biashara itahakikisha inaendelea kupambania viwanda kukua ili kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) amesema Wizara ya Viwanda na Biashara itahakikisha inaendelea kupambania viwanda kukua ili kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuona uwekezaji ukienda mbele.
Dkt.Jafo amesema hayo Mei 09,2025 Kimbiji-Kigamboni Dar es Salaam alipotembelea Kiwanda cha Lake Cement kinachozalisha bidhaa za Sarujii ya Nyati kwa lengo la kuangalia uwezo wa kiwanda na uzalishaji ili wananchi wapate bidhaa kwa bei nafuu, pia kumsaidia Rais Dkt.Samia kuwawezesha vijana kupata ajira kupitia kupitia sekta ya viwanda na biashara na kubaini changamoto walizonazo ili serikali izifanyie kazi.
Aidha Dkt.Jafo amesema ameona uzalishaji ukienda vizuri katika Kiwanda hicho na ukiongezeka kutoka tani 630,000 hadi milioni moja kwa taarifa za Mkurugenzi wa Kiwanda hicho hivyo amewataka Wakala wa Barabara wa Vijijini na Mijini (TARURA) kusaidia matengenezo ya kipande cha barabara cha Kimbiji- Mwasonga chenye urefu wa kilomita nane kikamilike ili mizigo inayozalishwa kupitia kiwanda hicho iweze kusafirishwa vizuri na kuchagiza ufanyaji biashara.
Aidha Dkt.Jafo amesema kiwanda hicho kimekuwa muhimu katika ukuaji wa uchumi kwa sababu kimekuwa kikichangia katika kutengeza ajira za moja kwa moja 335 na zisizo za moja kwa moja 300 kwa vijana pamoja na kodi ya serikalini ya zaidi ya sh.Bilioni 16 hivyo wakifanyabiashara vizuri mauzo yakiongezeka hata kodi itapanda.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa wilaya ya Kigamboni Bi.Pendo Mahalu amesema maelekezo ya Dkt. Jafo ameyachukua na kuyafanyia kazi ili kiwanda hicho kiongeze uzalishaji kwa wakati na kulinda ajira za Watanzania.