Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Ujenzi wa Jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo (WMA) jijini Dodoma


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwezesha ujenzi wa Jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo (WMA) jijini Dodoma akisema ni matumizi mazuri ya fedha za Watanzania.

Ameyasema hayo Januari 20, 2025 baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo hilo ambalo limegharimu shilingi bilioni 6.2 na liko katika hatua za mwisho umaliziaji.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dkt. Abdallah amesema kuwa lengo la ujenzi wa jengo hilo ni kuhakikisha utoaji huduma katika sekta ya Biashara hususan katika bidhaa zinazotoka viwandani unaboreshwa.

Dkt. Abdallah ameongeza kuwa maboresho ya kutoa huduma bora katika sekta ya Biashara na katika uendelezaji wa Viwanda ni pamoja na kuwa na mazingira mazuri kwa wafanyakazi na yale ya utoaji wa huduma hizo.

“Na katika hili, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo mengi makubwa, mojawapo ikiwa ni ujenzi wa jengo hili ambalo tunakwenda kulizindua hivi karibuni,” amesisitiza.

“Ninyi wenyewe ni mashahidi; fedha za Watanzania zinaenda kukamilisha ujenzi huu ili tuweze kutoa huduma bora katika jamii ya wafanyabiashara ili tuweze kuleta maendeleo na tija katika sekta ya viwanda,” ameongeza Katibu Mkuu.

Kuhusu mtazamo wake kutokana na maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, Katibu Mkuu Hashil ameeleza kuwa kwa mujibu wa maelezo na uthibitisho uliotolewa pamoja na kujionea kwa macho kazi inavyoendelea, ni dhahiri Mkandarasi atakamilisha kazi ndani ya muda ulioafikiwa ambao ni Februari 10, 2025.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, pamoja na kuunga mkono pongezi na shukrani kwa Rais Samia kuwezesha ujenzi wa jengo hilo, pia amebainisha kuwa ujenzi umefikia asilimia 95.2 na kwamba kukamilika kwake siyo tu kutaboresha mazingira ya wafanyakazi wa Wakala bali pia kwa Serikali kwa ujumla.

Akidadavua baadhi ya faida zitakazopatikana kutokana na kukamilika kwa jengo hilo, Mtendaji Mkuu ameeleza kuwa maabara ya kisasa ndani yake itawezesha kuhifadhi vifaa ambavyo kitaalamu vinajulikana kama vyenye usahihi wa kati au kwa lugha ya kigeni ‘secondary standards’