Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Utafiti wa Viwanda ni muhimu Uwezeshwe


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya  Viwanda, Biashara, Kilimo na Biashara  imeishauri Serikali kuongeza uwigo wa bajeti kwa wizara ya uwekezaji viwanda na biashara ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo hususani utafiti wa viwanda ambao ndio nguzo ya maendeleo ya uchumi wa viwanda nchini. 

Aidha, Kamati hiyo imeishauri Wizara hiyo kuweka Mipango Mikakati ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati na ya kielelezo huusani Mradi wa Liganga na Mchuchuma ili kutekeleza miradi hiyo yenye manufaa makubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya taifa kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati hiyo cha Machi 21, 2023 Mhe.  Mhandisi Ezra  Chiwelesa (Mb.) wakati  Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ikiwasilisha Taarifa  ya Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa Kamati hiyo katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Nao Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maoni mbalimbali yaliyolenga kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya miradi ya utafiti wa viwanda ambayo ni  muhimu katika maendeleo ya sekta ya viwanda ili yaendane na wakati, teknolojia ya kisasa na mahitaji ya sekta zote za uzalishaji ikiwemo kilimo na mifugo, uwezeshaji wa  wajasiriamali na utafutaji wa masoko ya nje ya bidhaa za Tanzania.

Akijumuisha,maoni na mapendekezo ya Kamati hiyo, Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara  Mhe. Dkt Ashatu Kijaji (Mb.) amesema Wizara itaendelea kutekeleza kikamilifu ushauri na maelekezo ya Kamati hiyo ili kuendeleza sekta ya uwekezaji, viwanda na biashara  na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Awali Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akiwasilisha Taarifa hiyo amesema kuanzia Julai 2022 hadi Febuari 2023, Wizara imefanikiwa kusajili jumla ya miradi mipya 204 yenye jumla ya dola za Marekani milioni 3,591 na kutoa ajira 31,531. 

Aidha, amesema Wizara imehamasisha ujenzi  na upanuzi wa viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo nchini ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za ndani, kukuza mauzo ya nje na kuzalisha ajira ikiwemo Viwanda vya Sukari  (Bagamoyo; Mkulazi, Kilombero na Kagera), Kiwanda cha Bia cha Serengeti Breweries – Moshi pamoja na Kiwanda cha mbolea cha Intracom Fertilizer Limited cha Dodoma na  Minjingu Arusha  ili kuleta tija katika kilimo.

Aidha amesema Wizara imeendelea kutekeleza Miradi ya Kimkakati na ya Kielelezo kwa manufaa ya Taifa ikiwemo Mradi wa Magadi  Soda - Engaruka, Makaa ya Mawe - Mchuchuma, Chuma - Liganga,  Chuma ghafi (iron ore) Maganga Matitu na Makaa ya Mawe -  Katewaka,  pamoja na ujenzi wa kongani za viwanda na maeneo maalumu ya uchumi ikiwemo  Kongani ya viwanda ya Kwala -Pwani, Mkulazi – Morogoro, Nala – Dodoma na Bagamoyo. 


Vilevile amesema  Wizara imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara, kuanzisha Mfumo wa Dirisha Moja la Kutoa Huduma kwa Wawekezaji, Kuendeleza Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, kuendeleza Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo na kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania na utekelezaji wa mikataba ya biashara