Habari
Utekelezaji wa MKUMBI kuvutia wawekezaji

Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Mazingira ya Biashara cha Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Bw. Baraka Aligaesha amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (MKUMBI) kwa kurekebisha sheria na kufuta tozo ada na fine ambazo zilikua kero kwa wafanyabiashara.
Ameyasema hayo wakati akishiriki mdahalo wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya lililofanyika tarehe 23 na 24 Februari, 2023 JNICC, Dar es Salaam.
Akiongea na Wawekezaji katika Kongamano hilo amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imerekebisha sheria 42 kati ya 88 zilizokuwa kero ikiwa ni sawa na asilimia 40, na hadi ifikapo 2024 sheria zilizobaki zitakuwa zimebadilishwa.
Pia, amesema ada faini na tozo 232 kati ya 380 zinazohusiana na masuala ya utawala na uzalishaji zimeshughulikiwa ili kuhakikisha mazingira ya biashara yanaboreshwa.
Aidha, akiwahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara hao mazingira bora aliongeza kuwa Serikali imeondoa baadhi ya majukumu yanayofanana kwenye mamlaka za udhibiti au kuunganishwa yale yanayofanana ili kurahisisha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa sekta binafsi.