Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wahariri wa vyombo vya habari nchini wana nafasi kubwa kupitia vyombo vyao kufanikisha ukuaji wa sekta ya biashara nchini.


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. amesema kuwa, wahariri wa vyombo vya habari nchini wana nafasi kubwa kupitia vyombo vyao kufanikisha ukuaji wa sekta ya biashara nchini.

Ameyamesema hayo leo Mei 21, 2022 kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu,Dkt.Hashil Abdallah katika kikao kazi cha siku mbili kati ya wahariri wa vyombo vya habari na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kinachoendelea mkoani Morogoro.

"Hivyo kwa muktadha huu niwaombe wahariri tushirikiane kwa pamoja kwenye kufanikisha ukuaji wa sekta ya biashara nchini, hasa wananchi wapate uelewa na warasimishe biashara zao. Amesema Dkt.Abdalah.

Pia Dkt. Abdallah amewaomba wahariri wanapotekeleza majukumu yao kutumia lugha rahisi kuwaeleza wananchi masuala ya BRELA na anaamini wahariri hao watakuwa mabalozi wazuri wa BRELA na watazibeba ajenda za wakala hiyo katika urasimishaji wa biashara ili wananchi waweze kupata taarifa njema ambazo zitawawezesha kunufaika kupitia wakala hiyo.

Katika hatua nyingine, Dkt.Abdalah amesema BRELA inapaswa kuendelea kuimarisha ushirikiano na vyombo vyote vya habari na kila wanapotakiwa kutoa ufafanuzi wa jambo fulani wasisite kufanya hivyo ili umma upate taarifa kwa haraka na kama habari wanayohitaji inachukua muda kupata majibu wapewe mrejesho mapema ili waweze kusubiri ili upotoshaji usiwepo.

"Mkumbuke kuwa, Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kila mtu-(a) ana uhuru wa kuwa na maoni na kujielekeza na kutoa maoni au mawazo yake, (b) ana haki ya kutafuta, kupokea na, au kusambaza taarifa bila kujali mipaka ya nchi,
"(c) ana uhuru wa kuwasiliana na haki ya kulindwa dhidi ya kuingiliwa kati ya mawasiliano yake, na (d) ana haki ya kupata taarifa wakatin wote kuhusu matukio mbalimbali yanayoendelea kuhusu maisha." Amesema Dkt.Abdalah.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, Bw.Godfrey Nyaisa amesema kuwa, usimamiaji wa majukumu ya msingi ya BRELA umewezesha kuwa na mafanikio makubwa yenye uwazi na ukuaji wa uchumi wa Tanzania hali ambayo inatokana na uboreshaji wa mazingira ya biashara na urahisishaji wa sajili na leseni.