Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wanawake,wajasiriamali wadogo wawezeshwa mikopo yenye riba nafuu .


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Mapinduzi Dkt.Ally Hassan Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitatu yenye thamani ya Euro million 270 kati ya taasisi za kibenki za Tanzania na Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya ambayo itawezesha watanzania hasa wanawake,wajasiriamali wadogo kupata mikopo yenye riba nafuu na kuwekeza kwenye uchumi wa buluu.

Akifunga kongamano la siku mbili la kibiashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya - EU Februari 24, 2023, Rais Mwinyi amesema Serikali ya Tanzania imejikita zaidi kutengeneza biashara ya ushindani hivyo anashukuru umoja wa Ulaya kwa kuchagua kuwezesha wafanyabiashara na kuwekeza kwenye uchumi wa buluu.

Aidha ameziomba nchi za umoja wa ulaya kushirikiana pamoja na Tanzania kutekeleza makubaliano yote walioyoyasaini kwa lengo la kukuza zaidi uchumi na biashara kwa pande zote mbili

Hata hivyo Miongoni mwa Benki zilizotia saini Hati za makubaliano ya kusaini Mkataba wa Euro milioni 270 ni pamoja na Benki ya CRDB, NMB na KCB ambapo wasimamizi wa benki hizo wameeleza kuwa mkopo huo ni rahisi kwani wakopaji hususani wanawake na vijana watalipa kwa muda mrefu kuanzia miaka miwili hivyo itawawezesha wafanyabiashara hao kuinua biashara zao huku wakiiomba EU  kuendelea kufanya  uwekezaji nchini.