Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wataalamu kutoka mamlaka za udhibiti biashara nchini kushiriki kikamilifu katika kuboresha rasimu ya Mwongozo wa kusajili, kuomba leseni na vibali vya kuendesha biashara nchini.


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara  Bw. Conrad Milinga kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara amewataka wataalamu kutoka mamlaka za udhibiti biashara nchini kushiriki kikamilifu katika kuboresha rasimu ya Mwongozo wa kusajili, kuomba leseni na vibali vya kuendesha biashara nchini.

Ameyasema hayo tarehe 13 Februari, 2023 alipofungua rasmi Mkutano wa  wadau wa Mamlaka za udhibiti biashara nchini wenye lengo la kuboresha rasimu ya muongozo wa kusajili, kuomba leseni na vibali vya kuendesha biashara nchini uliofanyika ukumbi wa bodi ya usajili ya wakandarasi Mkoani Dodoma.

Bw. Milinga amesema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuboresha mazingira ya biashara nchini.

“Kupitia mradi wa Business Environment Growth and Innovation (BEGIN) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) umeendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI) ambao umekuwa ukijulikana kama “BLUEPRINT” kwa sasa unaendelea na kazi ya kuchapisha Mwongozo wa kusajili, kuomba leseni na vibali vya kuendesha biashara nchini hivyo nyinyi ni wadau muhimu katika uandaaji wa rasimu hii, Amesema Bw. Milinga.

Awali akiwasilisha taarifa ya Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI), Mratibu wa Maboresho hayo Bw. Baraka Aligaesha amesema kuwa kazi kubwa ya kitengo cha kuboresha Mazingira ya biashara ni pamoja na kuangalia sheria, kanuni na taratibu pia kuangalia taasisi zenye muingiliano na mifumo ya kutoa huduma kama inakidhi na pia mifumo ya ukaguzi ambayo inaongeza gharama na muda.

“Kupitia MKUMBI umesaidia kuongeza uwezo wa kusajili makampuni ndani ya siku moja, vibali vingi vya kwenye mamlaka za udhibiti sasa vinatolewa kwa siku zisizo zidi tatu, hivyo mazingira ya biashara yameendelea kuboreka siku hadi siku na kwa kupitia mwongozo huu unaenda kuchochea ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu”. Amesema Bw. Aligaesha.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Sehemu ya Viwanda Vidogo na Biashara ndogo Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhandisi Charles Irege amesema kuwa lengo la kuzikutanisha taasisi za udhibiti biashara nchini ni kupitia rasimu ya Mwongozo huo kwa lengo la kurahisisha biashara na kuchochea kuongezeka kwa shughuli rasmi za kiuchumi na kupunguza sekta isiyo rasmi. 

Bw. Irege ameongeza kuwa mwongozo huo utasaidia kutoa taarifa muhimu kutoka taasisi za udhibiti juu ya ufanyaji wa biashara na kuondoa adha ya gharama na muda kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.