Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wawekezaji waliochukua viwanda vilivyobinafsishwa kwa nia ya kuwekeza wawekeze na si kuvigeuza kuwa magodauni


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb.) amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji- Msajiri wa Hazina itapanga utaratibu bora wa kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa na havifanyi kazi vinaendelezwa na kufanya kazi ili kuongeza ajira, pato la taifa na kukuza uchumi kwa ujumla.

Aidha, ameiagiza Wakala wa Vipimo (WMA) kugagua mita zote za umeme viwandani ili kuhakikisha zinafanya kazi kwa usahihi na wazalishaji, wafanyabiashara, walaji na TANESCO wanapata haki yao sawasawa.

Ameyasema hayo Agosti 22, 2024 wakati wa Ziara yake Mkoani humo ambapo alipotembelea viwanda na kuongea na Wafanyabiara na Wamiliki wa Viwanda kwa lengo la kujionea utendaji kazi, kusikiliza changamoto zao na kuona njia bora ya kuzitata kwa kushirikiana na Taasisi nyingine husika.

“Katika mkoa wa Tanga kuna viwanda vinavyofanya vizuri na vingine havifanyi vizuri. Hivyo Sijaridhishwa na viwanda vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi . Ninawashauri Wawekezaji waliochukua viwanda vilivyobinafsishwa kwa nia ya kuwekeza wawekeze na si kuvigeuza kuwa magodauni au kuwa sehemu ya kupata mikopo na kuwaacha Watanzania wakikosa ajira na pato la Taifa. “ Amesema Dkt. Jafo.

Aidha, amebainisha kuwa kwa kishirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekwzaji, Wizara ya Fedha, Msajiri wa Hazina pamoja na Taasisi za kisekta atahakikisha changamoto zilizotolewa zinafanyiwa kazi ili kurudisha hadhi ya Mkoa wa Tanga kama Mkoa wa Viwanda kama ilivyokuwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Kwa upande wa Changamoto ya umeme mdogo, Dkt Jafo amebainisha kuwa
Serikali imefanya jitihada kubwa kushughulikia changamoto hiyo na kuwa Mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) uko mbioni kukamilika na kuwa tatizo la umeme limeanza kupungua kwa kwa kiasi kikubwa.

Aidha katika ziara hiyo Waziri Jafo alitembelea Kiwanda cha sabuni cha Wilmar Tanzania Limited, Kiwanda cha nguo cha AFRITEX, Kiwanda cha Maziwa cha Tanga Fresh, Kiwanda cha unga cha Pembe Flour Mills na Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro.