Habari
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb,) aitaka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuratibu vyema sekta ya uwekezaji Nchini.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb,) aitaka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuratibu vyema sekta ya uwekezaji Nchini.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo tarehe 20 Aprili, 2023 alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki, kinachojengwa na Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center kwenye eneo la Ubungo, mtaa wa National Housing jijini Dar es Salaam.
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Januari, 2023 Serikali ilisajili jumla ya miradi ya uwekezaji 537 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 7,222 ambapo hatua hiyo imetokana na kuboreshwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kuimarisha Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja ili kuvutia wawekezaji kwa kupunguza kero na kurahisisha utoaji huduma.
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Mauzo ya Nje (EPZA) imefanikiwa kusajili Miradi 38 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 139.70 na mauzo nje yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 191.04.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Kituo hicho cha Biashara cha Afrika Mashariki kitakuwa na maduka zaidi ya elfu mbili, ambayo yatakuwa na ukubwa tofauti ili kukidhi mahitaji ya wafanyabishara wa aina zote na kupanua fursa ya Watanzania wengi kufanyabiashara katika eneo hili.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb,) amesema kuwa mradi huo una thamani ya dola za Kimarekani milioni 81.827 na kwa kupitia mradi huu utaifungua Tanzania kibiashara na kukuza uchumi kutokana na biashara zitakazokuwa zikifanyika na kukuza mahusiano ya Kimataifa kwa kuwa na muingiliano wa wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali na kupelekea upatikanaji wa ajira za moja kwa zaidi ya 15,000. na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 50,000.
Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara amesema kuwa kazi kubwa inayofanywa na Wizara ni kutafsiri kwa vitendo sheria, kanuni na falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC) Dkt. Cathy Wang amesema kuwa mapato ya jumla kwa mwaka yatafika zaidi ya dola za marekani milioni 500 pindi mradi huo utakapokamilika hivyo kusaidia katika ukuaji wa pato la taifa na kuongeza mapato ya kikodi.
Amesema kuwa mradi huo wa kimkakati ambao utakuwa moja ya mradi mkubwa ndani ya afrika mashariki utawezesha kukuza biashara ndogo nchini na kupanua biashara hizo ndani ya soko kubwa la Afrika ambapo Mradi huo utakuwa na maduka 2,060 yenye ukubwa wa jumla ya mita za mraba 75,000 ambapo eneo hilo litakuwa na huduma zote za kibiashara ikiwemo mabenki na huduma za ufungashaji na usafirishaji.