Habari
Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda Mhe. Dk Ashatu Kijaji (Mb.) ameliomba Bunge kupitisha bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 119.018 mwaka wa fedha 2023-2024

Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda Mhe. Dk Ashatu Kijaji (Mb.) ameliomba Bunge kupitisha bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 119.018 na kati ya hizo Sh 43.566 zinaombwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ambapo Sh bilioni 30.347 ni fedha za ndani na Sh bilioni 13.22 ni fedha za nje.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2023/24 katika ukumbi wa Bunge, Dodoma, Mei 4,2023, Dkt Kijaji amebainisha vipaumbele nane katika sekta ya biashara na uwekezaji vitakavyotekelezwa katika bajeti ya mwaka 2023/24.
Dkt. Kijaji ametaja vipaumbele hivyo vikuu kuwa ni pamoja na kutekeleza Miradi ya Kielelezo ya Magadi Soda Engaruka, Makaa ya Mawe-Mchuchuma na Chuma-Liganga na uwekezaji katika maeneo maalum ya kiuchumi (SEZ) na kongani za viwanda ikiwa ni pamoja na Nala SEZ, Kwala SEZ, Mkulazi SEZ, Eneo Maalumu la Uwekezaji Bagamoyo.
Dkt. Kijaji alisema pia wamepanga kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kuboresha mazingira ya biashara, kukuza uwezeshaji wananchi kiuchumi na kukuza sekta binafsi.
Amesema pia kuratibu majadiliano ya biashara baina ya nchi na nchi, Kikanda na Kimataifa na kuimarisha huduma za biashara na masoko.
Kuhusu malengo ya wizara kwa mwaka 2023/24
Dkt. Kijaji amesema Wizara imepanga kukamilisha maandalizi na kuanza kutekeleza Sera mpya na mkakati wake kuhusu uwekezaji, kuratibu uanzishaji na uendelezaji wa miradi mikubwa ya uwekezaji yenye manufaa mapana kwa Taifa na kuendelea kuratibu programu za uhamasishaji wa uwekezaji ndani na nje ya nchi.
Amesema pia kuratibu programu za kuimarisha mifumo ya udhibiti wa uwekezaji inayolenga katika kupunguza gharama za uwekezaji nchini na kuratibu kuratibu ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya uwekezaji.
Dkt. Kijaji amesema pia kuwa Wizara itaendelea kuratibu utatuzi wa migogoro na changamoto za uwekezaji, kuratibu uanzishwaji wa maeneo maalum ya kiuchumi, kuendeleza miradi ya kitaifa ya kielelezo ya Bagamoyo na Tanga.
Wizara imejipanga kukamilisha malipo ya fidia katika maeneo ya uwekezaji ya Bagamoyo, Tanga, Manyoni, Nala na Ruvuma na kuhamasisha uendelezaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi kupitia Soko la Mitaji. Amesema Dkt. Kijaji.
Pia Amesema Wizara imepanga kutafuta ardhi kwa ajili ya uwekezaji, kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala mbalimbali ya uwekezaji, kufanya tafiti za uwekezaji ili kuibua fursa za uwekezaji na kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Pia kushirikiana na Balozi za Tanzania katika kuitangaza Tanzania ili kuvutia uwekezaji kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania na kuunganisha taarifa za vivutio vya uwekezaji vinavyotolewa na taasisi mbalimbali za umma nchini.
Kwa upande wa uwezeshaji kiuchumi na maendeleo ya sekta binafsi, Dk Kijaji alisema Wizara imepanga kuratibu sekta binafsi ili iweze kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo
Kwa upande wa maendeleo ya viwanda, Dk Kijaji alisema Wizara imepanga kukamilisha Sera, Mikakati na Miongozo ya kuendeleza sekta ya Viwanda na kuboresha na kuongeza ustawi na tija ya viwanda nchini.