Habari
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) ametoa rai kwa wawekezaji na jumuiya za wafanyabiashara kutoka Kusini Mashariki mwa Asia
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) ametoa rai kwa wawekezaji na jumuiya za wafanyabiashara kutoka Kusini Mashariki mwa Asia kuwa na ushirikiano wa kimkakati na Wtanzania na Afrika kwa ajili ya kuzalisha ajira, kuboresha maisha ya watu na kwa ukuaji wa uchumi.
Ametoa rai hiyo wakati wa jukwaa la Biashara baina ya Tanzania,Afrika ma Kusini Mashariki mwa bara la Asia iliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Novemba 13, 2024.
Dkt.Jafo amesema Tanzania,imekuwa ikiamini katika nguvu ya ushirikiano kwa miaka mingi ma imeona uwezekano wa kufanya kazi na washirika wa Kusini Mashariki mwa Asia hivyo kongamano hilo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusioano huo ambao utaendeleza maisha ya baadae ni Malengo ya pamoja ya maendeleo ya kiuchumi, uendelevu, na uvumbuzi wa kiteknolojia.
Vilevile Dkt.Jafo amesema katika jitihada za kuimarisha uwekezaji nchini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameunda Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi, kwa ajili ya kupitia na kuishauri serikali kuhusu masuala ya kodi, kuunda upya sera ya Biashara ya mwaka 2023 na imeanzisha Dirisha la Uwekezaji wa Kielektroniki pamoja kutenga maeneo ya uwekezaji katika kila Mkoa,Wilaya na Halmashauri.
Pia amesema Tanzania inatoa fursa kubwa kwa wawekezaji hasa kutoka Kusini Mashariki mwa Asia, na kuzitaja sababu zinazofanya Tanzania iwe nchi ya kwanza kwa biashara barani Afrika ikiwemo kuwa Nchi ya kimkakati inayopatikana kando ya Bahari ya Hindi ambapo inafanya kama lango la kuingia katika nchi zisizo na bandari, uwekezaji katika miundombinu ya barabara, reli na nishati,kukua kwa Uchumi na sekta za kilimo, utalii, madini, uwepo wa maeneo maarufu ya utalii , Uwekezaji mkubwa wa nishati mbadala, ikiwemo nishati ya jua, upepo na maji, kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji kupitia vituo vya uwekezaji, Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs), na mageuzi ya kuboresha biashara pamoja na kupata fursa za soko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) ambalo Tanzania ni Mwanachama.