Habari
SERIKALI YADHAMIRIA KULINDA MILIKI UBUNIFU KUKUZA UCHUMI WA MICHEZO NCHINI
Serikali imedhamiria kulinda haki za miliki michezoni kwa kuwataka wadau wa michezo nchini kurasimisha na kulinda haki zao za Miliki Ubunifu ili kugeuza tasnia hiyo kuwa biashara yenye tija.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith Kapinga (Mb), Mei 08, 2026, jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA), huku akisema kuwa michezo imehama kutoka kuwa burudani pekee na sasa ni nyenzo muhimu ya uchumi inayotegemea maarifa na ubunifu.
Waziri Kapinga amebainisha kuwa ulinzi wa alama za biashara, hataza, na hakimiliki ni muhimu katika kulinda thamani ya timu, wachezaji, na wawekezaji na kuwa Serikali inafanya mageuzi makubwa ya kisheria na kisera ili kuhakikisha kazi za wabunifu na wanamichezo zinalindwa dhidi ya maharamia, hali itakayosaidia kuongeza mapato ya vilabu na Serikali kwa ujumla.
Aidha, Waziri Kapinga ametoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na uzalishaji na uingizaji wa bidhaa bandia, hususan jezi za timu za michezo, akieleza kuwa kitendo hicho kinadhoofisha uchumi wa vilabu.
Waziri Kapinga amesisitiza kuwa Serikali iko tayari kuendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuchochea uvumbuzi na kutoa rai kwa viongozi wa mashirikisho ya michezo kuwaongoza wachezaji wao kulinda haki za taswira na picha zao (image rights), akibainisha kuwa miliki ubunifu ni rasilimali inayoweza kuishi na kunufaisha vizazi hata baada ya maisha ya mbunifu mwenyewe, hivyo ni lazima itunzwe kwa wivu mkubwa.
Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Aristides Mbwasi kwa Niaba ya Katibu Mkuu alimshukuru Waziri wa Wizara hiyo kwa maono na maelekezo yake katika kutimiza adhma ya Serikali.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela Bw. Godfrey Nyaisa amesema Milki Bunifu ni Nyenzo muhimu ya utambulisho wa nchi mbele ya walaji au watumiaji wa bidhaa.
