Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wito watolewa kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani kuzingatia ubora ili ziweze kushindana katika soko.


NaibuWaziriwa Viwanda na Biashara,Mhe. Exaud Kigahe (Mb) ametoa wito kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani kuzingatia ubora ili ziweze kushindana katika soko.

Mhe. Kigahe ameyasema hayo Februari 23,2025 alipotembelea kiwanda cha kutengeneza Chaki kilichoko Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu alipofanya ziara ya kutembelea na kujionea uzalishaji wa bidhaa hiyo kiwandani hapo.

Mhe. Kigahe amefurahishwa na shughuli zinazofanywa na kiwanda hicho kinachomilikiwa na Halmashauri ya wilaya hiyo na kusema kuwa ni kiwanda kikubwa ambacho Serikali imeamua kuwekeza kwa gharama ya sh. bilioni 10

“Bilioni 10 zimewekezwa katika kiwanda hiki ili uwekezaji uwe na tija ni vizuri kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitashindana na bidhaa nyingine kwenye soko la nje,”

Amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sio kufanya biashara bali kuendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji na wafanyabiashara ndani na nje ya nchi na ndiyo maana Halmashauri ya Wilaya hii imeamua kuanzisha  kampuni ya Nghami Industries Company Ltd ili iweze kusimamia kiwanda hicho.

Pia amewataka wafanyakazi wa kiwanda hicho kuwa mstari wa mbele katika kukisemea vyema pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kujenga ufanisi lakini wakati huo huo ametaka kuboreshwa kwa vitendea kazi kwa wafanyakazi hao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw.Maisha Mtipa amesema kuwa kuanzia mwezi Mei 2024 hadi Januari 31,2025 uzalishaji wa chaki vipande 2,529,147 vimeweza kutoa katoni 843.05 na katoni 250 zimeuzwa.

Amesema kuwa mapato baada ya kutoa gharama za uendeshaji yanatarajia kufikia Sh 16.3 bilioni kwa miaka kumi na tano na kwa mwezi ni Sh 3 bilioni.

“Mapato ya kiwanda hiki yatatusaidia kutekeleza miradi yetu ya maendeleo katika halmashauri yetu kupitia mapato ya ndani kwani tulikuwa tukitegemea sana zao la pamba kama ndicho chanzo kikuu cha mapato yetu ya ndani,”amesema.