Habari
Wizara ya Madini na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara zimeazimia kuanza utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati

Wizara ya Madini na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara zimeazimia kuanza utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati ikiwemo Liganga na Mchuchuma, Maganga Matitu, Katewaka na Magadi soda kwa haraka ili kuleta tija kwa wananchi waishio maeneo hayo na taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallaha akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Bwana Kheri Mahimbali katika kikao kilichofanyika Machi 9, 2023 Mtumba jijini Dodoma kilicholenga kujadili Miradi hiyo ya Kimkakati.
Akizungumza katika kikao hicho,
Dkt. Abdallah amesema Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara itashirikiana kwa karibu na Wizara ya Madini katika kutekeleza miradi hiyo ya kimkakati kwa haraka ili kuhakikisha inaleta tija katika maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Naye Bw. Mahimbali amesema, miradi hiyo itatekelezwa kwa wakati ili rasilimali hizo zilinufaishe taifa na watanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara muda wote inapohitajika ili shughuli za utekelezaji wa miradi hiyo uweze kuanza kama ilivyopangwa.