Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Ziara ya Naibu Waziri kutembelea kongano la usindikaji wa mafuta ya Alizeti.


Naibu Waziri, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (Mb) amefanya ziara ya kikazi ya siku ya jumamosi tarehe 15 Sept, 2018 katika Mkoa wa Singida kwa kutembelea Kongano la usindikaji mafuta ya Alizeti la Mtinko. Kongano ili lilianza mwaka 2013 kwa uhamasishaji wa Viwanda kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, SIDO, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida na Halmashauri ya Singida ili kuwa na kongano bunifu la mfano kwa ngazi ya Wilaya. Kongano la Alizeti Singida lenye ukubwa wa hekari 6.6 lina wanachama 66, kati ya hao 30 ni wanaviwanda na waliobakia ni wakulima, wafanyabiashara na wasafirishaji. Katika hotuba yake Naibu Waziri, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (Mb) ameanza kwa kuwapongeza SIDO Mkoa wa Singida, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halmashauri ya Wilaya ya Singida pamoja na wataalamu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kufanikisha uanzishwaji wa Kongano hilo. Aidha Mhe. Naibu Waziri amewapongeza wadau wa maendeleo ambao ni JICA waliosaidia ujenzi wa chumba cha maabara na Vifaa vya maabara, MIVARF na MEDA. Mhe. Naibu Waziri amewaagiza taasisi za TFDA na TBS kukamilisha taratibu za kitaalamu haraka ili wazalishaji hawa wa kongano la Mtinko kupata vibali ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora wenye viwango, Naibu Waziri pia amekabidhi majembe 23 kwa wakulima wa Alizeti, majembe hayo yametolewa kwa wakulima ambao watalipia asilimia 50 na asilimia 50 inayobaki italipwa na wafadhili. Mhe. Naibu Waziri amehitimisha ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha uzalishaji wa mafuta ya Alizeti cha Yaza Investment Company Ltd kilichopo eneo la ndago Mkoani Singida, pia amempongeza ndugu ndugu, Yusuph Amri Nalompa ambaye ni mtendaji mkuu wa kiwanda kwa ubunifu wa kuanzisha kiwanda hicho kusaidia wakulima wa alizeti mkoani Singida na pia kutengeneza ajira, Mhe. Naibu Waziri amemuhakikishia ndugu, Yusuph Amri Nalompa ushirikiano kutoka serikalini na changamoto anazopata zitashughulikiwa kwa haraka zaidi.